MAHAKAMA ya wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, imemtia hatiani na
kumhukumu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe kwenda jela
mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh milioni moja, kutokana na kesi
iliyokuwa ikimkabili ya kumshambulia mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2010.
Akisoma hukumu hiyo iliyohudhuriwa na wabunge wengi wa Chadema, Hakimu
Mkazi Mfawidhi, Denis Mpelembwa, alisema mahakama imemkuta Mbowe na
hatia, hivyo kutakiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela au kulipa
faini kiasi cha Sh milioni moja.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Hai, katika kesi hiyo ya jinai
namba 73 ya mwaka 2011, alidaiwa kumshambulia Nassir Yamin, katika
Kijiji cha Nshara, kata ya Machame Kaskazini, Wilaya ya Hai, katika
uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Mpelembwa alisema mahakamani hapo kuwa hukumu iliyotolewa mahakamani
hapo imezingatia ushahidi uliotolewa kwa upande wa mlalamikaji Nassir
Yamini.
Kwa upande wake, Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe akizungumza mahakamani
hapo, alisema hukumu iliyosomwa mahakamani hapo haijamtendea haki.
Alisema kesi yake hiyo haikustahili kuchukua muda mrefu kama mahakama
ilivyofanya kwa kuchukua zaidi ya miaka mitano bila kusomewa hukumu.
Hata hivyo, Mbowe amelipa kiasi cha fedha Sh milioni moja alichotakiwa
kulipa kama hukumu ilivyoeleza, kwa kumtaka kulipa kiasi hicho cha fedha
au kwenda jela mwaka mmoja.

No comments:
Post a Comment