Watu 10 wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro baada ya kukamatwa
msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera nyeusi
inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab wa nchini
Somalia.
Katika tukio hilo, mmoja anayesadikiwa kuhusiana na watu
hao waliokamatwa aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya kumjeruhi kwa
panga askari polisi aliyekuwa akipambana naye.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo, Kamanda wa polisi mkoani Morogoro, Leonald Paul
alisema tukio hilo limetokea jana (Aprili 14) majira ya saa 3.30 usiku
katika kitongoji cha Nyandero, tarafa ya Kidatu wilayani
Kilombero.Kamanda Paul alimtaja mtu aliyefariki kuwa ni Hamad Makwendo
ambaye umri wake haujafahamika ambaye ni mkazi Manyasini Ruaha wilayani
Kilombero.
Aidha alisema siku ya tukio polisi walipata taarifa
kutoka kwa raia wema kuhusu watu hao na kwamba walitaarifiwa kuwa
wanajihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu na polisi waliamua
kufatilia nyendo zao.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Paul alisema: “Polisi walipata taarifa
kuwa watu hao walitumia usafiri wa bajaji mbili kwenda kusikojulikana
na wakati wakiendelea na zoezi la kufuatilia ndipo walikutana na bajaji
moja ikiwa na abiria mmoja ambaye ni Mkwendo na kuisimamisha.”
Alisema
kuwa bajaji hiyo iliposimama marehemu huyo aliruka na kuanza kukimbia
ndipo askari mwenye namba F .3323 Koplo Nasoro alianza kumkimbiza na
alipomkaribia mtuhumiwa huyo alichomoa jambia alilokuwa nalo na kumkata
askari huyo eneo la shingoni.
Askari mwingine mwenye namba E.9245
Koplo Chomola ambaye alikuwa nyuma alifanikiwa kumpiga risasi ya mguu
mtuhumiwa huyo, ambapo alipoanguka chini wananchi wa eneo hilo tayari
walifika katika eneo hilo na kuanza kumshambulia marehemu huyo kisha
kumchoma moto kwa hasira.
Kamanda huyo alisema walianza kuwasaka watu wengine ambao walipata taarifa wapo katika Msikiti wa Suni uliopo Kidatu.
“Polisi
walipofika katika msikiti huo waliuomba uongozi wa msikiti huo kuwatoa
watu wote waliokuwa msikitini ili kuweza kubaini watu ambao wanatiliwa
mashaka.”
Alisema polisi walendelea na ukaguzi na kuwakamata watu hao 10 wakiwa na vifaa hivyo na kuwatia nguvuni.
No comments:
Post a Comment